Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga Samwel Lukamay na aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji, akishikilia nyadhifa za Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano na Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Hussein Nyika, wamejiuzulu nafasi zao leo Machi 27, 2019.
Nyika na Lukumay wametangaza hilo, kwenye makao makuu ya klabu hiyo ambapo wameweka wazi kuwa wamefanya hivyo ili kupisha uchaguzi utaowezesha klabu kupata viongozi wapya.
Wawili hao ndio waliokuwa wamebaki kwenye uongozi wa Yanga ambao uliingia madarakani mwaka 2016 baada ya wengine kujizulu, hivyo sasa timu hiyo inabaki bila uongozi mpaka pale uchaguzi mkuu utakapofanyika.
''Ninajiuzulu nafasi zangu zote nikiwa kama Mjumbe wa kamati ya utendaji lakini pia Mwenyekiti wa kamati ya usajili na kamati ya mashindano na niombe msamaha kwa wale niliowakosea katika utekelezaji wangu wa majukumu'', amesema Nyika.
Kwa upande mwingine Lukumay ameeleza kuwa wameamua kufanya hivyo ili kutoa nafasi kwa uchaguzi mkuu kupata viongozi wote tofauti na awali ambavyo ilikuwa ni uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi.
Aidha Lukumay amesema timu inakabidhiwa kwa wanachama kupitia kwa Baraza la Wadhamini la klabu hiyo ambalo lipo chini ya Mwenyekiti George Mkuchika.
Hivi karibuni Baraza la wadhamini la Yanga liliweka wazi kuwa, badala ya kufanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizowazi ikiwemo ile ya Mwenyekiti, utafanyika uchaguzi mkuu kwaajili ya kupata viongozi wote