Ubalozi wa Uswisi nchini umetoa Sh bilioni 18 kwa asasi za kiraia tatu, zitakozotumika kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Fedha hizo zinalenga kusaidia asasi hizo katika shughuli zao za kuboresha uwazi na uwajibikaji kwenye nyanja mbalimbali nchini. Asasi zilizonufaika na fedha hizo ni Foundation for Civil Society (FCS), Policy Forum na Twaweza.
Akizungumza kwenye shughuli ya kutiliana sahihi ya msaada huo, Balozi wa Uswisi nchini Florence Mattli ameeleza kuwa lengo kuu la msaada huu ni kushiriki katika kukuza uwajibikaji kwenye mamlaka mbalimbali, ili kuboresha sera na huduma za jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza Aidan Eyakuze ameeleza kuwa msaada huo utasaidia taasisi hizo kuendeleza ushirikiano baina yao na serikali.
“Asasi nyingi za kiraia zina mawazo mazuri lakini hazina uwezo wa kuwasilisha mawazo hayo kwenye ngazi husika, msaada huu utatusaidia kuwafikia na kuwawezesha kuwasilisha mawazo ya wananchi,” aliongeza