VITA BARIDI: Rais Kagame afunguka chanzo cha mgogoro wa Rwanda na Uganda, adai ni bifu la miaka 20
0
March 15, 2019
Rais wa Rwanda, Paul Kagame amefunguka kwa mara ya kwanza chanzo cha mgogoro uliopo kati ya taifa lake na nchi jirani ya Uganda, kwa kueleza kuwa mgogoro huo sio wa jana bali ni wa miaka 20 iliyopita na ulisukwa kwa lengo la kuangusha utawala wake.
Image result for kagame vs museveni
Rais Museveni na Kagame
Akihutubia mkutano wa kitaifa wa Umwiherero unaofanyika kila mwaka nchini humo, Kagame amesema mgogoro huo umeshika kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na serikali ya Uganda kuunga mkono kundi la RNC , linalopinga Serikali ya Rwanda na ambalo linatumiwa na Uganda kuwanyanyasa raia wa Rwanda wanaotembelea au wanaoishi nchini Uganda.
Akihutubia kwenye mkutano huo unaohudhuriwa na watu takribani 250 wakiwemo viongozi wakuu serikalini na wawakilishi wa vyama vya wafanyabiashara, Rais Paul Kagame alirejelea maandiko ya kitabu kinachoitwa ‘From Genocied to continental War” ambacho kiliandikwa na mwandishi maarufu wa vitabu kutoka Ufaransa, Gerard Prunier .
Rais Kagame amesema mwandishi huyo, aliandika kuwa alikutana na waziri wa zamani wa mambo ya ndani, marehemu Seth Sendashonga mnamo mwaka 1998 pamoja na maafisa wakuu wa jeshi la Uganda na kuzungumzia mipango ya kumsaidia Sendashonga ili kuangusha utawala wa Kagame.
Mwandishi huyo katika kitabu chake kulingana na maelezo ya Rais Kagame, Uganda ilikuwa imemuahidi kumsaidia kijeshi.
”Sababu ya mimi kurejelea kuzungumza haya nimetaka kuwaonyesha mfululizo wa jinsi mambo yalivyokwenda mnamo miaka 20 iliyopita.“ameeleza Kagame.
Kagame amesema kwa kipindi chote hicho cha miaka 20, amekuwa akichukua hatua mbalimbali kupata suluhisho la mgogoro huo lakini ilishindikana.
“Tulijaribu kufanya mikutano ya hapa na pale ili kutafuta suluhu. lakini matatizo hayo hayakuisha. Kuna kipindi nilituma watu hadi kwa Mwenzangu (Rais Museveni) lakini hakutilia maanani. Ukweli ni kwamba Seth Sendashonga alifariki dunia kwa kuwa alivuka mstari mwekundu. Sifurahii kusema hivyo lakini pia sijutii kifo chake.”ameeleza Kagame kwenye mkutano huo.
Seth Sendashonga aliuawa mwaka 1998 Nairobi nchini Kenya, katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa uhamishoni baada ya kutofautiana na Serikali ya Rwanda.
Rais Kagame amesema mgogoro huo umeshika kasi siku za hivi karibuni, hii nikutokana na raia wa Rwanda wanaoishi na wanaoingia nchini Uganda kushikwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani na kuteswa.
Kagame ameituhumu serikali ya Uganda kuwa inatoa ushirikiano kwa kundi la Rwanda National Congress (RNC) linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda Jenerali Kayumba Nyamwasa, ambalo hadi sasa linapinga serikali ya Kagame.
”RNC wanafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya Uganda. Wanachokifanya ni kunyanyasa wanyarwanda ambao hawataki kuungana nao, huku wakiwasingizia kwamba wametumwa na utawala wa Kigali kuhujumu usalama wa Uganda na kuuwa wanyarwanda wa upinzani. Ni madai yasiyo na msingi,lakini haya yote yanaonyesha ushirikiano wa dhati uliyopo baina ya serikali ya Uganda na kundi la RNC.”ameeleza Kagame.
Kwa upande mwingine wa shilingi, Uganda imekuwa ikiishutumu Rwanda kuwa inatuma majajusi nchini mwake kupepeleza masuala ya usalama, jambo ambalo serikali ya Rwanda imekanusha.
Wiki iliyopita, serikali ya Rwanda ilikataza wananchi wake kwenda nchini Uganda na kusababisha mkwamo wa biashara kati ya mataifa hayo jirani.
Rwanda inasema inatoa kipaumbele kwa maisha ya Raia wake zaidi, kuliko biashara baina ya nchi hizo mbili.
Serikali ya Uganda nayo jana ilitoa taarifa ya kukanusha kuzuia malori kutoka Rwanda kuingia nchini humo. Na badala yake imeeleza kuwa Rwanda ndio imezuia Malori ya Uganda kutoingia nchini humo isipokuwa yale yanayoenda DR Congo.
Tags