Wanawake CHADEMA, CCM wanusurika kuzichapa


Katazo la Jeshi la Polisi Wilaya ya Geita la kuwazuia wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kuadhimisha Kitaifa siku ya Mwanamke Duniani Katika Mkoa wa Geita nusura lizue vurugu kubwa mkoani humo.

Hiyo ni baada ya baadhi ya wakereketwa na viongozi wa Umoja wa wanawake(UWT) Mkoa wa Geita kuonyeshwa kukerwa na hatua ya wanawake wa CHADEMA kujumuika pamoja nao kwenye viwanja vya soko jipya kata ya Kalangalala kama walivyoamuliwa na Jeshi la polisi.

Katazo hilo limetolewa Machi saba mwaka huu, na Jeshi la Polisi Wilaya ya Geita likiwazuia  wanawake wa CHADEMA kufanya maadhimisho ya siku ya mwanamke Kitaifa katika Mkoa huo kupitia barua yenye yake yenye kumbukumbu GE/B.3/24/VOL.VII/63 na kusainiwa na Alli Kitumbu, Mkuu wa Polisi wilaya.

Kutokana na hali hiyo,wanawake na wanachama wa CHADEMA na viongozi mbalimbali wa kitaifa waliokwishawasili mkoani humo, walilazimika kuungana na wenzao kwenye viwanja hivyo kwa ajili ya kusherehekea siku hiyo jambo lililozua minong’ono ya hapa na pale kutoka kwa baadhi ya wafuasi wa CCM na kuvilazimu vyombo vya ulinzi na usalama kuwa na wakati mgumu kuwatuliza.

Baada ya hali ya utulivu kurejea, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita aliyekuwa Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, alitoa salamu za Serikali ya awamu ya tano na kusema kuwa  imejipanga kuondoa changamoto zinazomkabili mwanamke.

Naye Mbunge wa viti maalumu kupitia CHADEMA, Upendo Peneza ameeleza namna anavyojitahidi kuwawakilisha vyema wanawake akiwa bungeni.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad