Waliopandishwa kortini ni Hamisi Mohamed (30), Mohamed Said (45), Alex Kyandarula (28) na Hamza Mohamed (24) wote wakazi wa Mbagala, Dar es Salaam.
Wakisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Frank Moshi, Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Abudi Yusuph alidai kuwa Januari 29, mwaka huu eneo la Mbezi Makabe, Wilaya ya Ubungo, washtakiwa waliiba runinga moja aina ya Hisence yenye thamani ya Sh 2,300,000 mali ya Sayana Juma ambaye kabla na baada ya kuiba walimtishia kwa panga ili kuijipatia mali hiyo.
Aidha mahakama hiyo imemsomea shtaka la pili mtuhumiwa wa nne la kukutwa na mali ya wizi.
Akisoma shtaka hilo, mwendesha mashtaka alidai kuwa Februari 2, mwaka huu eneo la Mbagala Rangi Tatu, Wilaya ya Temeke, mshtakiwa alikutwa na runinga aina ya Hisence mali ya Sayana Juma ambayo ndiyo iliyoibwa huko Makabe.
Washtakiwa walikana kutenda kosa hilo huku upande wa Jamhuri ukisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa.
Hakimu Moshi alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa namba nne aliyetakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria ambao watatoa bondi ya Sh 500,000.
Mshtakiwa alikidhi masharti ya dhamana na kuachiwa huku washtakiwa watatu wakirudishwa rumande kutokana na shtaka lao kutokuwa na dhamana hadi kesi yao itakaposomwa tena Machi 18, mwaka huu.