Watu saba wamehukumiwa kwenda jela miaka mitatu wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza na mahakama ya kutembea (mobile court) kwa kosa la kufanya uvuvi haramu, huku wengine 14 wakifikishwa katika mahakama hiyo kwa kosa hilo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa operesheni hiyo, Ofisa Mfawidhi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi, Kanda ya Ziwa Didas Mtambalike, alisema wameamua kuboresha utendaji kazi dhidi ya kudhibiti uvuvi haramu kwa kutembea na mahakama ikiwa ni sehemu ya kurahisisha hukumu kwa wahalifu na kuondoa msongamano wa kesi mahakamani.
Mtambalike alisema ndani ya siku 10 wamefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa 14 na kati yao saba wameshasomewa hukumu yao ya kufungwa miaka mitatu jela kila mmoja au kulipa faini ya shilingi milioni tatu na wote walishindwa kulipa fedha hiyo na kwenda kutumikia kifungo gerezani kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2009.
Aidha, alisema kikosi chake kimekamata makokoro ya sangara 60, vipande vya makila vilivyounganishwa 1,385, nyavu za dagaa 60, ndoano 4,700, pikipiki 35 na injini 17, huku kikosi cha halmashauri hiyo kikiwa kimekamata makokoro 48 ya sangara, 41 ya dagaa, nyavu za makila 870, ndoano 3,200, baiskeli 20 na pikipiki tano, jumla vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. milioni 500.