Waziri Aagiza Kuongezwa Dalala 10 Kusaidia Mabasi ya Mwendokasi Dar

Waziri Aagiza Kuongezwa Dalala 10 Kusaidia Mabasi ya Mwendokasi Dar
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ameagiza kuongezwa kwa mabasi 10 ya kawaida katika usafiri wa mwendokasi jijini Dar es Salaam ili kupunguza changamoto ya usafiri.

Jafo alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika kituo cha mwendokasi cha Kivukoni na kuzungumza na abiria kuhusu changamoto wanazokutana nazo katika usafiri huo wa mabasi ya mwendokasi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Jafo alisema usafiri huo wa mwendokasi umekuwa ukisuasua jambo ambalo halimfurahishi ikizingatiwa kwamba wananchi wengi wamekuwa wakiutegemea.

Alisema tatizo hilo limekuwa likijitokeza mara kwa mara na kusababisha usumbufu kwa wananchi na mpaka sasa hajaona njia stahiki na ya kuridhisha zilizochukuliwa na watoa huduma katika kupata ufumbuzi changamoto hiyo.

“Tatizo hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika kituo cha mabasi cha Kimara wakati wa asubuhi na Kivukoni na Gerezani wakati wa jioni. Imeonekana pia kuna wakati mabasi yanaonekana yakisafiri tupu au yakiwa yameegeshwa pembeni mwa vitu, huku abiria wakiwa wamejazana katika vituo vya mabasi,” alisema.

”Kutokana na hali hiyo namwelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi Dar es Salaam (Dart), Mhandisi Ronald Lwakatare, ahakikishe angalau mabasi 10 ya Feeder Road maarufu kama Bomberdier yanayobeba abiria kutoka Mbezi kwenda Kimara Mwisho yahamishiwe katika barabara ya mwendokasi. Matano yawe yanabeba abiria wa Kivukoni na matano mengine yabebe abiria wa Gerezani,” aliongeza.

Jafo alisema milango ya mabasi hayo hairuhusu kupakia katika vituo vya mabasi ya mwendokasi ya kawaida, hivyo mabasi hayo yatachukua abiria moja kwa moja kutoka Kimara hadi Kivukoni au Gerezani na wakati wa kurudi Kimara yatachukua abiria wanaoshuka Kimara pekee.

Aidha, Jafo alitoa maelekezo ya Dart kuwasiliana na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ili mabasi ya kawaida yaongezwe kwa eneo la Kimara mpaka Mbezi ili abiria watakaoshuka Kimara wakitokea katikati ya Jiji kwenda Mbezi na wale watakaotoka Mbezi kwenda Kimara wapate usafiri wa haraka.

“Namwelekeza Mtendaji Mkuu wa Dart, Mhandisi Lwakatare, ahakikishe Udart ambayo ndiyo kampuni yenye dhamana ya kusafirisha abiria ihakikishe inafanya matengenezo ya mara kwa mara ya mabasi yake ili kuondoa usumbufu unaojitokeza wa upungufu wa mbasi kutokana na mabasi mengi kuwa mabovu,” alisema.

Jafo alimtaka Lwakatare awasilishe kwa Katibu Mkuu wa Tamisemi majina ya watendaji walio chini yake ambao anahisi hawasaidii ipasavyo kiushauri na kiutendaji ndani ya siku saba ili wafanye marekebisho kwa maslahi mapana ya Taasisi ya Dart.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad