Wizara zote zinazohusika na Vyama vya Ushirika kwa Akiba na Mikopo (SCCULT) zimetakiwa kuhakikisha kwamba zinakuwa na dawati la Ushirika na taarifa zake kuwasilishwa kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania.
Pia, Tume ya Maendeleo ya Ushirika imetakiwa kuhakikisha kuwa inasimamia, kudhibiti na kuhamasisha Vyama vya Ushirika viweze kufanya kazi kikamilifu na kwa wakati kwa kuzingatia Sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015; na kanuni za Vyama vya Ushirika wa akiba na mikopo ya 2014.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameyasema hayo wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye kongamano la Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Afrika linalofanyika mkoani mwanza katika ukumbi wa Malaika Beach Resort leo tarehe 27 Machi 2019.
Hasunga alisema kuwa mamlaka zote zinazohusika na Maendeleo ya Sekta ya Ushirika nchini zijiwekee malengo yanayotekelezeka ya kusukuma gurudumu la Maendeleo ya ushirika na kujipima kila mara.
Kadhalika Serikali imesema kuwa itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wote wanaobainika kuhujumu dhamira njema ya maendeleo ya
ushirika kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na matarajio ya kuanzishwa kwa vyama hivyo.