Waziri Kabudi awapa moyo Zimbabwe 'Msiba wenu ni msiba wetu'

Waziri Kabudi awapa moyo Zimbabwe 'Msiba wenu ni msiba wetu'
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi amesaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Zimbabwe ulioko jijini Dar es Salaam na ambapo mpaka sasa takribani watu 179 wamepoteza maisha na wengine wakiwa hawajulikani waliko kutokana na kimbunga Idai kilichosababisha mafuriko nchini humo.

Akizungumza katika Ubalozi wa Zimbabwe jijini Dar es Salaam mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo ubalozini hapo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba John Kabudi amemtaka Kaimu Balozi wa Zimbabwe hapa Nchini Bw Martin Tvenyika kufikisha salam za rambirambi kwa serikali na watu wa Zimbabwe kwa maafa yaliyotokea na kwamba serikali ya Tanzania iko pamoja na wananchi wote wa Zimbabwe katika kipindi hiki kigumu cha maafa.

“Msiba wenu ni msiba wetu na matatizo yenu ni matatizo yetu na kama nilivyosema ninyi na sisi chimbuko letu ni moja na tumekuwa pamoja tangu katika harakati za kutafuta uhuru kwa hiyo mioyo ya mababu zetu ambayo imetuweka pamoja kwa miaka yote hii iendelee kuwatunza,kwani ziko hadithi na mapokeo kwamba washona na wabena ni walewale hivyo sisi ni ndugu na Mwenyezi Mungu awasaidie wale wote waliopatwa na misiba”

Kaimu Balozi wa Zimbabwe Nchini Tanzania Bw Martin Tvenyika ameishukuru serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na kubainisha kuwa hadi kufikia jana taarifa zinasema takribani watu 179 wamethibitika kufariki dunia na wengine wakiwa hawajulikani walipo huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.

“Maji yanapozidi kupungua ndivyo miili mingi inavyozidi kupatikana na kwa kweli tunashukuru sana kwa msaada mnayotupatia kwani imekuwa ya manufaa sana. Ni ukweli kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kutoa msaada wa haraka wa kiutu ikiwemo chakula na dawa na Rais wetu Comrade Emmerson Mnangagwa anatoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwa hatua hii ni moja ya mifano mingi ya mahusiano mazuri ya muda mrefu na ya kindugu yaliyopo baina ya Tanzania na Zimbabwe”

Kaimu Balozi wa Zimbabwe, Bw Martin Tvenyika ameyataja maeneo yaliyoathirika zaidi na kimbunga cha Idai kuwa ni Chimamani na Manica land lililoko Mashariki mwa nchi ya Zimbabwe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad