Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke mapema hii leo Machi 13, 2019 katika ofisi zake Jijini Dodoma
Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa ni kujadili maeneo muhimu yanayohusu masuala ya uwekezaji ambapo Waziri Kairuki alieleza vipaumbele muhimu vya uwekezaji vitakavyochangia adhma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ikiwemo kuwekeza katika maeneo ya kilimo, elimu, afya, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi wa Miundombinu ya barabara.
“Ninafarijika kwa ujio wako na ni ishara nzuri ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili naamini yatasaidia katika fursa za uwekezaji hasa kwa namna Uingereza ilivyochangia katika maeneo muhimu nchini ikiwemo elimu,”alisema Kairuki
Waziri aliongezea kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuzingatia mchango unaotokana na wawekezaji hasa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.
Waziri Kairuki alieleza kuwa, kuwepo kwa Idara ya uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ni hatua muhimu kwani itasaidia kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa masuala hayo na kuendelea kuleta mabadiliko katika kutatua changamoto zilizozikabili sekta hiyo.
Aidha alimshukuru balozi huyo kwa hatua ya mazungumzo yenye tija pamoja na kuendelea kuunga mkono nchi ya Tanzania na kuwataka kuendeleza urafiki huo kwa kuwekeza zaidi katika maeneo aliyoyaainisha ikiweko yale ya vipaumbele.
Naye Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania, Sarah Cooke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na sera zinazovutia wawekezaji pamoja na maboresho yanayofanywa kuwavutia wawekezaji nchini ikiwemo maeneo ya ulipaji wa kodi.
“Tunaelewa kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na mazingira ya ulipaji wa kodi tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwa na mchango katika maendeleo ya nchi pamoja na kuimarisha mahusiano yaliyopo,”alisisitiza Cooke.
Waziri Kairuki Akutana Na Kufanya Mazungumzo Na Balozi Wa Uingereza Nchini
0
March 13, 2019
Tags