Waziri Lugola Apiga Marufuku Polisi Jamii Kukamata Bodaboda na Askari Polisi Kukamata Vyombo Vya Moto Bila Kuvaa Sare Za Jeshi

Waziri Lugola Apiga Marufuku Polisi Jamii Kukamata Bodaboda na Askari Polisi Kukamata Vyombo Vya Moto Bila Kuvaa Sare Za Jeshi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku Polisi jamii kukamata bodaboda zinazofanya makosa ya usalama barabarani nchini.

Pia Waziri huyo amepiga marufuku polisi wa usalama barabarani kukamata vyombo vya moto wakiwa hawajavaa sare za Jeshi.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Mafisa, Kata ya Mwembesongo, mjini Morgoro, jana, Lugola alisema Polisi Jamii hawana ujuzi wa kijeshi wa ukamataji wa bodaboda hivyo kuendelea kuifanya kazi hiyo ni kuwanyanyasa wananchi.

“Nimepata malalamiko mengi ninapofanya ziara zangu hapa nchini, wengi wanawalalamikia Polisi Jamii kuwaonea, kuwaomba rushwa na kuwakamata pasipofuata utaratibu unaotakiwa kijeshi, hapa Morogoro pia, katika mkutano huu wa hadhara mnayasema yale yale, sasa natangaza kuanzia leo, marufuku Polisi Jamii kukamata bodaboda,” alisema Lugola.

Waziri Lugola pia alipiga marufuku baadhi ya Polisi wa Usalama barabarani ambao wenye tabia ya kutovaa sare za Jeshi na kuingia barabarani au mitaani na kuyakamata magari na bodaboda.

Lugola alisema lazima polisi wafate sheria za usalama barabarani hasa wanapokamata magari yanayofanya makosa, uvaaji wa sare za Jeshi ni muhimu na unapaswa kufutwa.

Waziri Lugola aliongeza kuwa, bodaboda au vyombo vingine vya moto, zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biashara hiyo.

“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha bodaboda,” alisema Lugola.

Lugola alifafanua kuwa, bodaboda zinazotakiwa kuwepo kituo cha polisi ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.

“Bodaboida hizo ndizo zinapaswa kuwepo vituoni, lakini kuziweka bodaboda ambazo hazipo katika makundi hayo, napiga marufuku na hii nataka Polisi nchi nzima munielewe,” alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Morogoro na Tanzania kwa ujumla wafate sheria za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.

Lugola ameanza ziara yake ya siku tatu mkoani humo akitembelea Wilaya za Morogoro, Mvomero, Kilosa na Gairo akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.

Lugola mwaka jana alitoa maagizo kwa makamanda wa mikoa nchini ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.

Waziri Lugola amemaliza ziara Wilaya ya Morogoro na leo ataanza ziara yake katika Wilaya ya Movemero, na Machi 10, 2019 atamalizia Wilaya ya Gairo ambapo katika Wilaya hizo pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad