WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Mwanza ihakikishe inafanya msako wa watu wote waliohusika na wizi wa fedha na vifaa katika eneo la ujenzi wa mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika mji wa Misungwi mkoani Mwanza.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Machi 19, 2019) wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira uliopo wilayani Misungwi, ambapo ametumia fursa hiyo kuiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Mwanza iimarishe ulinzi katika eneo la mradi huo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa ya kuwepo kwa vitendo vya uvamizi wa mara kwa mara kwenye eneo hilo la mradi wa maji unaojengwa katika kijiji cha Nyahiti wilayani Misungwi, Mwanza.
“Hawa waliofanya tukio hilo la uvamizi katika eneo la mradi si tu wanamuhujumu mkandarasi na kampuni yake, bali wanahujumu jitihada za Serikali ili miradi ya maendeleo kwa wananchi isikamilike hatutakubali, wananchi tushirikiane katika kuwabaini wote waliohusika.”
Ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Misungwi ni utekelezaji wa Sera ya Maji pamoja na Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020 inayoelekeza Serikali kuwapatia huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 95 wakazi waishio mijini na waishio vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.
Awali,Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Misungwi unatekelezwa kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Viktoria, ambao unatekelezwa katika miji ya Mwanza, Musoma, Bukoba, Magu, Misungwi na Lamadi kwa gharama ya Euro milioni 104.5 sawa na wastani wa sh. bilioni 276.
Amesema katika kiasi hicho cha fedha, Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) zinachangia Euro milioni 90 sawa na sh. bilioni 238 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu, ambapo Serikali ya Tanzania inachangia Euro milioni 14.5 sawa na sh. bilioni 38.
Profesa Mbarawa amesema mradi wa maji na usafi wa mazingira katika mji wa Misungwi unagharimu kiasi cha Euro milioni 4.85 ambazo ni sawa na wastani wa sh. bilioni 12.85 ambazo zinatumika katika ujenzi wa kituo cha uzalishaji na kutibu maji, ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 53.7.
Pia, fedha hizo zitatumika kwenye ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ukubwa wa lita 600,000 na lita 300,000, ujenzi wa kituo cha kutibu majitaka, ununuzi wa magari mawili moja la kunyonya majitaka na Toyota pick up na pikipiki mbili pamoja na ujenzi wa ofisi ya Mamlaka ya Maji na nyumba mbili za watumishi katika kituo cha uzalishaji.
Waziri Profesa Mbarawa amesema mbali na ujenzi huo pia watajenga maabara ya kupima ubora wa maji na karakana ya matengenezo. Mradi huo pia utaunganisha kaya 2,158 katika mfumo wa maji pamoja na kuwafungia mita za maji na ujenzi wa vituo 13 vya kuchotea maji.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC) ya China chini ya Mhandisi Mshauri Kampuni ya Egis ya Ufaransa na unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Jijini Mwanza (MWAUWASA) ulianza Mei, 2017 na unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu.
Waziri Mkuu Aagiza Msako Kwa Waliomuibia Mkandarasi Misungwi
0
March 20, 2019
Tags