Waziri Ummy Mwalimu Akemea Waajiri Sekta Binafsi Wanaofukuza Kazi Wanawake Pindi Wapatapo Mimba

Serikali imeagiza taarifa za waajiri wote hasa sekta binafsi waliowafukuza wanawake kazi au kuwashusha vyeo kwa sababu ya kupata ujauzito wakiwa kazini.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitoa agizo hilo jijini hapa wakati akizungumza na wanawake na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Aliitaka jamii katika maeneo ya kazi kuondokana na rushwa za ngono jambo alilosema ni tatizo katika upatikanaji wa haki za wanawake.

Kadhalika aliwataka waajiri wa sekta binafsi kuzingatia utu na haki za wanawake wafanyakazi.

"Mwanamke kupata mimba ni haki yake ya asili kutokana na uumbaji wa Mungu hivyo ni marufuku kuwafukuza kazi wanawake wafanyakazi hasa sekta binafsi kisa kuwa na ujauzito," alionya.

Aliongeza kuwa suala la usawa wa kijinsia ni muhimu kwa wanaume kushiriki kwa kuwa wao pia ni wahusika wakuu wa kuwapo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Waziri Ummy alisema kama waziri mwenye dhamana ya masuala ya wanawake atahakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika masuala muhimu kwa manufaa ya haki na ustawi wao.

Aliagiza kutekelezwa kwa haki ya mwanamke kunyonyesha baada ya kumaliza likizo zao za uzazi, kwa kuwa ni jambo muhimu kwa mtoto kupata maziwa ya mama katika ukuaji wake kwenye umri wa miezi ya awali.

Waziri Ummy alikemea vitendo vya rushwa ya ngono na kuipongeza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kuliona suala hilo kuwa moja kati ya vitendo vya kikatili afanyiwavyo mwanamke na kumnyima haki yake.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Philis Nyimbi, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, alisema mkoa unatekeleza mikakati mbalimbali katika kumwezesha mwanamke na mtoto wa kike kwa kumuweka mbali na vitendo vya ukatili dhidi yao ili kuwawezesha kupata fursa zitakazowezesha kufikia usawa wa kijinsia.

Naye Mwakilishi Mkazi Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez, alisema kuwa Umoja wa Mataifa unataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha kunakuwapo na usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo vyote vinavyosababisha kutokuwapo kwa usawa wa kijinsia kama vile mimba na ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikiwanyima fursa watoto wa kike kutimiza ndoto zao.

Alisema kuwa mapambano ya usawa wa kijinsia yatafanikiwa pale yatakaposhirikisha wanaume na wavulana katika kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata fursa sawa katika kutimiza ndoto zao.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake UN Women, Hodan Addou, alisema kuwa shirika hilo linashirikiana na serikali na mashirika ya kitaifa kuhakikisha elimu inatolewa na usawa wa kijinsia inakuwa suala la kipaumbele katika jamii.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad