Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi Asikitishwa na Taasisi za Kimataifa Zinazoishutumu Serikali Kabla ya Kuifata Itoe Ufafanuzi

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya “Defend Defenders” Bw. Hassan Shire na Bw. Nicolas Agostini.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Geneva nchini Uswisi wakati wa Kikao cha 40 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kinachofanyika Mjini Geneva ambacho Prof. Kabudi anahudhuria.

Prof. Kabudi na viongozi wa Taasisi hiyo wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu nchini ambapo pia walimkabidhi Prof. Kabudi Ripoti yao ya mwaka 2018 ambayo iliishutumu Serikali kwa ukiukwaji wa masuala mbalimbali ya haki za binadamu.

Akizungumza na viongozi hao, Prof. Kabudi alieleza masikitiko yake kwa Taasisi hiyo na Taasisi nyingine kwa kuishutumu Serikali na kutoa ripoti na taarifa mbalimbali ambazo zinatoa shutuma dhidi ya Serikali bila kuwasiliana na Serikali ili kupata ufafanuzi wa shutuma hizo.

Alisema vitendo hivyo vinasababisha upotoshaji mkubwa wa hali halisi ya masuala ya haki za binadamu nchini na jitihada za Serikali katika kutekeleza wajibu wake wa kukuza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu.

Prof. Kabudi alisisitiza umuhimu wa taasisi hiyo na taasisi mbalimbali kuishirikisha Serikali ili kupata maelezo kutoka  pande zote na kupata uelewa wa jambo kabla ya kutoa taarifa zao ambazo zinaishutumu Serikali.

Amesema Tanzania kama nchi nyingine inapata changamoto mbalimbali wakati inatekeleza jukumu yake la kulinda, kuheshimu na kukuza haki za binadamu nchini na pale inapoonekana kuwa haitekelezi ipasavyo wajibu iliyonao ni vizuri mashauriano yakafanyika na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa wajibu wa kulinda na kustawisha haki za binadamu kwani mawasiliano yangefanyika ripoti hiyo isingetoka hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya “Defend Defenders” alikiri kuwa hawakuwasiliana na Serikali kabla ya kutoa ripoti hiyo, na alimshukuru Prof. Kabudi kwa kuridhia kukutana nao na kwamba Taasisi hiyo imepokea ushauri ya Mhe. Waziri na kuahidi kuendelea kujadiliana na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ambayo inasimamia masuala ya haki za binadamu.

Waziri Kabudi alitumia fursa hiyo kuukaribisha uongozi wa Taasisi hiyo Tanzania ili wapate ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo yameripotiwa kuhusu Tanzania na kama ina maoni au mapendekezo kuhusu namna bora ya kuboresha haki za binadamu nchini wanakaribishwa kujadiliana na Serikali  kupitia Wizara ya Katiba na Sheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad