Baraza la Wadhamini la Klabu ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake George Mkuchika, limependekeza klabu hiyo isifanye uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizowazi kwa sasa badala yake wafanye uchaguzi mkuu ili kupata viongozi wapya.
Akiongea leo Machi 13, 2019 baada ya kikao cha kamati ya utendaji na Baraza la wadhamini Mkuchika amesema wameazimia kuwaomba wanachama kufanya uchaguzi wake mkuu mwaka huu 2019 badala ya mwaka 2020.
Mkuchika ameitaja sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kupisha uchaguzi mkuu wa nchi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2020.
''Maamuzi haya tunayepeleka kwa wanachama wote na wajumbe wa mkutano mkuu kwani sio busara kujaza mapengo mwaka huu kisha tena mwakani tufanye mkutano mkuu wa uchaguzi, tunaita mkutano wa wanachama wote ili wakikubali hili lifanyike kwa ridhaa yao isijekuonekana sisi tuwaburuza'', amesema.
Aidha amesisitiza kuwa jambo hili la kuwashirikisha wajumbe wa mkutano mkuu ili wapitishe pendekezo hilo linatakiwa kufanya haraka ikiwezekana ndani ya wiki tatu au nne.