Kocha mpya wa Real Madrid, Zinedine Zidane anaanza kazi leo baada ya jana kutangazwa rasmi kuchukua mikoba ya Santiago Solari, aliyefukuzwa.
Zidane anarejea Madrid, miezi 10 baada ya kuipa ubingwa wa Ulaya mara 3 mfululizo, akiwa na kibarua kigumu cha kurejesha makali ya timu hiyo iliyoondolewa katika michuano ya klabu bingwa Ulaya na Ajax kwa kipingo cha aibu cha 4-1. Katika ligi kuu ya Hispania "Laliga" Madrid kwa sasa iko katika nafasi ya tatu ikiizidiwa pointi 12 na vinara wa ligi hiyo Barcelona.
Zidane amepewa kandarasi ya miaka mitatu na nusu kuwanoa mabingwa hao wa kihistoria wa Ulaya, na mara baada ya kutambulishwa rasmi mbele ya wanahabari, Zidane,46, anasema ana furaha kurejea nyumbani.
"Nataka kuirejesha klabu hii pale ilipokuwa, ni ngumu sana kujua yanayoendelea ukiwa nje nimekuwa nikiishi Madrid, na kufanya mambo yangu hapa lakini sasa nimepata nguvu mpya, niko tayari kuiongoza klabu hii tena." alisema Zidane
Rais wa Madrid, Florentino Perez amemtaja Zidane kama mmoja wa makocha bora duniani.
"Kocha bora duniani amerejea kuungana nasi, malengo yetu ni kuwa wamoja tena."