Baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania kukipa chama cha ACT-Wazalendo wiki mbili kujitetea kwa nini wasifutiwe usajili wao wa kudumu, Kiongozi wa ACT Zitto Kabwe ameibuka na kutoa kauli.
Kwa mujibu wa barua kutoka ofisi ya msajili, ilidai vitendo vya uvunjifu wa sheria vilivyojitokea wakati wa hama hama ya wanachama wa CUF kwenda ACT ni miongoni mwa sababu za kutoa kusudio la kukifungia chama cha ACT.
“Kumezuka vitendo vya uvunjifuwa Sheria ikiwemokuchoma moto bendera za chama za CUF, vinavyofanywa na mashabiki wa Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, ambao wanadai sasa ni wanachama wa ACT-Wazalendo. Kitendo cha kuchoma moto bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C cha Sheria ya Vyama vya Siasa,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Msajili pia amedai kuwa kupitia mitandao ya kijamii, kuna video inayoonesha watu wakipandisha bendera ya ACT kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbira). Kitendo hicho, kwa mujibu wa msajili kinavunja vifungu 9(1)(c) na 9(2)(a) vinavyokataza kuchanganya shughuli za vyama vya siasa na dini.
Sababu nyengine iliyotajwa na msajili ni ACT kushindwa kuwasilisha ripoti ya hesabu za fedha za chama kwa mwaka 2013/2014.
Kiongozi wa ACT Zitto Kabwe ameiambia BBC Swahili kuwa hoja zote za msajili hazina mashiko na wataandika utetezi rasmi kama walivyotakiwa.
Zitto amesema sheria inawataka kuhakikisha wanachama wao hawavunji sheria na si watu baki, “…kama ilivyoandikwa kwenye barua ya Msajili, wale ambao wamefanya vitendo hivyo si wanachama wetu. Hatuna wajibu nao.”Kuhusu taarifa ya ripoti ya hesabu za chama kwa mwaka 2013/2014 Zitto amesema taarifa hizo zilijumuishwa kwenye hesabu za mwaka 2014/2015. “ACT ilianzishwa miezi miwili kabla ya mwaka wa fedha (2014/15) kuisha, hivyo kiuhasibu na kama tulivyoshauriwa na Mkaguzi, tulijumuisha hesabu hizo za miezi miwili katika hesabu za mwaka uliofuatia 2014/2015.”
ACT wanatarajiwa kuwa na mkutano wa dharura leo na baadae Zitto ataongea na waandishi wa habari kuanzia saa tano asubuhi.
Zitto afunguka sakata la ACT Wazalendo kufutiwa usajili wa kudumu
0
March 26, 2019
Tags