Ziwa Manyara Hatarini Kutoweka Serikali Yaashauriwa Kuweka Mikakati Madhubuti

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeshauri Serikali kuandaa mpango Mkakati wa haraka wa kunusuru Ziwa Manyara ambalo liko hatarini kutoweka kutokana shughuli za kibadamu.

Akizungungumza kwa niaba ya Kamati yake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Murad Sadick amesema ni wakati muafaka sasa jambo hili kupewe kipaumbele ili kunusuru hali ya sasa inayotishia uhai wa ziwa hilo.

Wakiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Manyara, Kamati hiyo imetembelea Ziwa Manyara na kujionea kupungua kwa kina cha maji kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo kisicho endelevu hususan katika vyanzo vya maji kinachopelekea ziwa hilo kujaa tope pamoja na ongezeko la mimea vamizi.

“Sote tumejionea hali halisi, hali ni mbaya, mimi na Kamati yangu tunawajibu wa kuishauri Serikali, hatua za haraka na za maksudi kunusuru hali hii, hata kwa maziwa mengine pia kama Ziwa Jipe na Ziwa Chala. Endapo hatua za haraka hazitachukuliwa ndani ya miaka kumi ijayo Ziwa hili litatoweka. Ikumbukwe kuwa ziwa hili ni chanzo kikubwa cha kukuza pato la Taifa kupitia Utalii hapa nchini” Alisisitiza Mhe. Sadick.

Akiwasilisha hatua za zilizochukukuliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuhusu kunusuru ziwa hilo Naibu Mkurugenzi Bw. William Mwakilime amesema kuwa Ofisi yake imechukua hatua za makusudi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya namna bora ya kuwa na kilimo endelevu kinachozingatia matumizi bora ya ardhi na kujenga mabwawa maalumu kwa ajili ya kuchuja maji.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muugano na Mazingira Mheshimiwa January Makamba alieambatana na Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge katika ziara hiyo, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha andiko jumuishi litakalogusa sekta zote kwa kuwa ni suala mtambuka na kuahidi kuwa Serikali inalipa uzito jambo hilo kwa mustakabali wa nchi na ustawi wa wananchi wake.

Katika hatua nyingine Kamati imeipongeza Serikali kwa kupokea ushauri wa Kamati hiyo ya kuunda kikosi kazi cha kupambana na mimea vamizi ambayo imekuwa ikiathiri maeneo mengi hapa nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Hifadhi. Waziri Makamba ameainisha kuwa Kikosi kazi hicho kilichoundwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais kimekamilisha kazi na taarifa yake iko katika hatua za maamuzi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iko katika ziara ya kikazi Mkoani Arusha pia itatembelea miradi ya uchimbaji wa visima Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ikiwa ni miongoni mwa miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais chini ya Mkataba wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad