Askofu Shoo: Kuna watu wanaotumia nguvu nyingi kuuficha ukweli bila kujua kuwa ukweli una asili ya kutofichika.

Askofu Shoo: Kuna watu wanaotumia nguvu nyingi kuuficha ukweli bila kujua kuwa ukweli una asili ya kutofichika.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT) Dkt Fredrick Shoo, amesema siku hizi duniani kuna watu wanaotumia nguvu nyingi kuuficha ukweli, bila kujua kuwa ukweli una asili ya kutofichika.

Askofu Dkt. Shoo, alitoa kauli hiyo jana wakati akihubiri kwenye ibada ya Pasaka iliyosherekewa duniani kote jana.

"Tunaweza kusema tunaipenda nchi yetu, lakini swali kubwa kwetu ni je tunao ujasiri wa kujitoa kweli kweli hata kiasi cha kutoogopa vikwazo vya hatari?" Alihoji Askofu Shoo.

Alisema ujasiri peke yake bila upendo unaotoka moyoni, huzaa ukatili na ujasiri usiokuwa na upendo huzaa hofu, na inapotokea kusimama kwa ajili ya wengine kwa manufaa ya wengine upendo bila ujasiri unabakia kuwa upendo wa mdomoni tu.

Aliongeza kuwa imefika hatua baadhi ya Wakristo wanaweza kusema wanampenda Yesu, lakini inapokuja saa ya kusimama kama shahidi wa Kristo, kuitetea familia yake, Kanisa na hata nchi yao, watu wanaingia mitini.

"Akina mama wale hawakusaliti, walisimama kweli kweli, na upendo wao huu wa dhati,î alisema Askofu Shoo. Aliongeza kuwa; "Ujasiri wa kujitoa kwa ajili ya wengine na familia, Kanisa na nchi unahitaji watu kama hawa wenye upendo wenye ujasiri na upendo wa kujitoa kwa ajili ya wengine"

Aliongeza kuwa wakati wa Yesu, askari waliokuwa wakilinda kaburi, walipewa pesa nyingi ili kuuficha ukweli, lakini haikuwezekana na leo wapo watu ambao wanajaribu kuwazuia Wakristo kutangaza habari za Yesu na kulizuia kanisa kufanya kazi ya Kitume, bila kujua kuwa tendo hilo ni la Mungu mwenyewe.

"Kulifanyika jitihada nyingi kwa ajili ya kuficha ukweli wa Yesu
kufufuka, askari walioshuhudia lile tetemeko na kushuhudia Yesu kufufuka walikuwa na hofu kubwa, walipewa pesa nyingi na wale wakuu wao, ili eti waseme Yesu hakufufuka, bali wanafunzi wake walikuja kumuiba usiku wakiwa wamelala."

"Lakini haikuwezekana kuuficha ukweli huo, habari za kufufuka kwa Yesu zikaenea na tena mbaya zaidi hata habari kwamba wakuu waliwapa pesa wale askari ili wanyamaze nazo zikaenea.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad