Rais aliyepinduliwa madarakani na jeshi nchini Sudan Omar al-Bashir yupo gerezani baada ya kukamatwa Jumanne usiku. Bashir aling’olewa madarakani wiki iliyopita katika mapinduzi ya kijeshi jijini Khartoum baada ya kuiongoza nchi yake kwa miaka 30.
Mwandishi wa BBC nchini Sudan ameongea na vyanzo ndani ya familia ya Bashir ambao wamethibitisha kuwa kiongozi huyo mwenye miaka 75 amekamatwa na kupelekwa jela.
Shirika la habari la kimataifa la Reuters linaarifu kuwa Bashir anashikiliwa kwenye gereza lenye ulinzi mkali la Kobar mjini Khartoum.
Kwa mujibu wa Reuters, al-Bashir anashikiliwa kwenye chumba cha peke yake gerezani na kuzungukwa na ulinzi mkali.
Kiongozi huyo alikuwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi nyumbani kwake toka alipopinduliwa wiki iliyopita.
Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan
Image captionLuteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan ndiye mkuu wa baraza la mpito la kijeshi linaloongoza Sudan
Nchi ya Sudan kwa sasa ipo chini ya uongozi wa Baraza la Mpito la Kijeshi chini ya Luteni Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan.
Katika hotuba kwenye televisheni siku ya Jumamosi, Jenerali Burhan aliapa “kuung’oa utawala”, na kuahidi kuheshimu haki za binaadamu, kusitisha marufuku ya kutotoka nje, kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, kuvunjilia mbali serikali zote za majimbo, kuwashtaki waliowaua waandamanaji na kukabiliana na rushwa.
Baraza hilo limewakamata baadhi ya waliokuwa maafisa wa serikali na kuahidi kutowatawanya waandamanaji.
Msemaji mmoja pia aliuomba upinzani kumchagua waziri mkuu mpya na kuahidi kumuidhinisha watakayemchagua.
Waandamanaji Sudan
Image captionWaandamanaji Sudan wanataka jeshi liachie hatamu za madaraka kwa uongozi wa kiraia
Katika mkutano na waandishi habari siku ya Jumapili, msemaji wa baraza Meja Jenerali Shams Ad-din Shanto ameeleza kwamba baraza la kijeshi lipo “tayari kuidhinisha” serikali yoyote ya kiraia itakayoidhinishwa na vyama vya upinzani.
“Hatutomteua waziri mkuu. Watamchagua,” alisema akimaanisha upinzani na makundi yanayoandamana.
Ameeleza pia kwamba jeshi halitowaondoa waaandamanaji kwa lazima lakini ametoa wito kwa waandamanaji hao “kuruhusu maisha yaendelee kama kawaida” na waache kuweka vizuzi kinyume cha sheria.
Baada ya Kupinduliwa Omar al-Bashir Aswekwa Gerezani, Sababu Zaelezwa
0
April 18, 2019
Tags