Akizungumza kabla ya kusaini mkataba wa makubaliano wa ujenzi wa jengo hilo, kati ya Wizara yake na Suma JKT ambayo iliongozwa katika kikao hicho na Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Martin Busungu, katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, iliyopo Mji wa Serikali, Kata ya Mtumba, jijini Dodoma, leo, alisema hana shaka na uwezo wa Mkandarasi huyo, ila anaamini ujenzi huo utakua bora na utakamilika kwa wakati.
“Baada ya maandalizi ya ujenzi huu kuchukua muda mrefu lakini hatimaye tumekamilisha, hivyo nawaomba ndugu zangu tufanye kazi vizuri kabisa, na leo ndio siku ya kusaini mkataba kwa ajili ya ujenzi huu,” alisema Meja Jenerali KIngu.
Meja Jenerali Kingu alisema Wizara yake itafuatilia kwa karibu ujenzi huo, ambapo Mkandarasi ni Suma JKT na Mshauri Elekezi ni Chuo Kikuu cha Ardhi, hivyo jengo hilo anatarajia kuwa bora zaidi kutokana na uwepo wa wadau hao.
Kwa upande wake, Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Busungu, alisema aliishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuwa na imani na Suma JKT na kuipa kazi ya ujenzi wa jengo la makao makuu ya uhamiaji jijini Dodoma.
“Tunaishukuru Wizara yako kwa kutupa kazi hii ya ujenzi wa jengo hili ambalo ni la ghorofa nane, tunaahidi kulikamilisha baada ya miezi 18, na tutapiga kadiri inawezekana, tupo tayari kwa kazi yenye uweledi wa kuzingatia muda na ubora ambao utawauza zaidi Suma JKT,” alisema Meja Jenerali Busungu.
Mkataba huo ulisainiwa na viongozi hao huku ukishuhudiwa na wanasheria wa taasisi hizo ambao ni Mkurugenzi wa Sheria, Marlin Komba wa Wizara hiyo na Kapteni Joyce Mwaikofu kutoka JKT.