Maafisa wa ngazi za juu katika utawala uliong'olewa madarakani wa Omar al-Bashir nchini Sudan wamepigwa kalamu nyekundu huku baadhi yao wakitiwa mbaroni.
Baraza la Kijeshi la Mpito linaloongoza nchini Sudan kwa sasa limetangaza kuwa, maafisa hao wamefukuzwa kazi huku wengine miongini mwao wakitiwa mbaroni, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza masharti ya shakhsia na viongozi walioandaa maandamano ya kumng'oa madarakani Omar al-Bashir.
Msemaji wa baraza hilo amesema mabalozi wa Sudan mjini Washington na Geneva ni miongoni mwa watu waliotimuliwa kazini katika mageuzi haya mapya.
Haya yanajiri huku serikali ya mpito ya Sudan ikiendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa mrengo wa mabadiliko walioongoza maandamano hayo.
Harakati ya Taifa ya Mabadilko (NFC) imetoa masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kubadilishwa muundo wa taasisi za kiusalama pamoja na kuvunjwa vikosi vyote vya wanamgambo wa utawala uliopinduliwa wa Jenerali Omar al Bashir vikiwemo vikosi vya ulinzi wa raia na polisi jamii.
Jana Jumapili, wananchi wa Sudan waliendeleza maandamano yao kulishinikiza Baraza la Mpito la Kijeshi la nchi hiyo likabidhi madaraka kwa raia haraka iwezekanavyo.
Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeiomba jamii ya kimataifa iliunge mkono Baraza la Mpito la Kijeshi kwa lengo la kuwepesisha mchakato wa makabidhiano ya uongozi kwa njia za kidemokrasia.