Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Dkt Maulid Madeni amefikia uamuzi wa kumshusha cheo Mkuu wa Kituo cha Afya cha Ngarenaro, Japhet Kivuyo, kwa kosa la kutokuwepo kazini siku ya pasaka kwa kile alichokidai alikuwa mapumzikoni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi huyo amesema kitendo kilichofanywa na mkuu huyo wa kituo kilikuwa kinyume na utaratibu wa utendaji kazi.
"Ofisi yangu inafanya uchunguzi na itachukua hatua stahiki, pia tunatoa taarifa kwa umma kuwa tunamvua uongozi Dkt Japhet Kivuyo kuwa Daktari wa kawaida, na nafasi yake itachukuliwa na Daktari David Mng'anya, mwisho tunawaomba radhi wananchi walioathirika kwa hili", amesema Mkurugenzi.
"Siku ile ya tukio ambayo ilikuwa Ijumaa, Daktari yule alitoa majibu ambayo si ya kiuongozi kwa sababu huwezi ukaondoka kwenye kituo cha afya, halafu hujaacha mbadala wowote, halafu unapigiwa simu unatoa majibu kwamba hauwezi kurudi ofisini", ameongeza Mkurugenzi huyo.
Mwishoni wa wiki iliyopita Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Wilayani Arusha, ilifanya ziara katika Kituo cha Afya cha Ngarenaro na kukuta wagonjwa wakiwa peke yao bila daktari yoyote wa kuwahudumia