Msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic amesema wataalamu hao wanachunguza hasi na hatari ya ugonjwa huo kusambaa kimataifa. Profesa Robert Steffen wa jopo la wataalamu wa afya wa UN anatazamiwa kutoa tangazo hilo.
Wakati huohuo, watu wanne zaidi wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mlipuko wa Ebola huko Kongo DR. Vifo hivyo vipya viliripotiwa katika maeneo ya mashariki mwa nchi.
Siku chache zilizopita, Wizara ya Afya ya Kongo DR ilitangaza kuwa, katika muda wa wiki tatu zilizopita, ugonjwa wa Ebola umeua zaidi ya watu 100; na zaidi ya watu 700 wamefariki dunia tangu mwezi Agosti Mosi mwaka jana kutokana na ugonjwa huo hatari.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, tangu homa ya Ebola iliporipuka nchini humo mwezi Agosti mwaka jana 2018 hadi sasa, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa au wanaoshukiwa kuambukizwa imefikia 1,206 , na 764 kati yao wamefariki dunia.
Shirika la Afya Duniani limetahadharisha kuwa, mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola unasambaa kwa kasi nchini Kongo DR, ikiwa ni miezi minane sasa tangu ulipoanza kugunduliwa tena kwa mara ya pili.