Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Taasisi ya BMVSS ya India zinatarajiwa kuendesha upimaji na kutoa bure zaidi ya miguu bandia 600 kwa watakaohitaji.
Watu wenye uhitaji wa miguu hiyo wametakiwa kufika MOI ndani ya mwezi huu kwa ajili ya vipimo na maelekezo mengine na kwamba ugawaji wa miguu hiyo utafanyika Mei, mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, alitoa wito huo jana na kusema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa MOI na serikali wa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora kwa wakati kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi.
"Ni azima yetu MOI na serikali kuhakikisha huduma zote zinawafikia wananchi hususani wa kipato cha chini, hivyo miguu hii bandia itatolewa bure kwa watu wenye uhitaji. Tunafahamu wako Watanzania wengi ambao walishindwa kupata miguu hii bandia kutokana na kukosa fedha, hivyo tumeona ni vyema tukawaondolea changamoto hii," alisema Dk. Boniface.
Alisema wako Watanzania wengi ambao wameshindwa kuendelea na maisha yao ya kila siku ya uzalishaji kwa kukosa miguu bandia.
Madaktari bingwa wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu wa MOI wamepiga kambi katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza na ambako watafanya upasuaji kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.