Hivi Shishi Food ya Shilole Imechakazwa na Mariam Birian?
0
April 26, 2019
KAZI ipo na waliotaka kazi wanapewa dubleduble. Wanahenyeshwa, wanatamani kuomba poo! Dar es Salaam ina mambo alisema Sugu kwenye wimbo Dar es Salaam. Na baba yangu aliniambia nikichelewa kufa nitaona mengi.
Nayaona mimi Luqman! Biashara ya chakula nilizoea kuona ikitangazwa kwa yale mapishi yake, ladha yake au hata mwonekano wa chakula chenyewe. Siku hizi ni tofauti. Maakuli yanatangazwa kupitia kiwiliwili cha mpishi. "Karibuni biriani tamu," mpishi anatangaza mitandaoni huku akijizungusha kuonesha neema za uumbwaji wake.
Mpishi anatangaza: "Mariam biriani ndiyo habari ya mjini. Karibuni sana Ijumaa hii." Baada ya maneno hayo anajizungusha, anajitembeza kwenye kamera. Kideoni mitandaoni anaonesha kile ambacho Sheikh Hilal Kipozeo huita "neema za Allah." Basi watu hoi! Mariam Biriani amekuwa habari nzito somo!
Unaambiwa hata wasiopenda biriani wamefunga safari kutoka Kiburugwa mpaka Kinyerezi kufuata biriani la Mariam. Bwa Shee alinishangaza kutoka Kishimundu mpaka Tabata kufuata biriani la Mariam. Nikamuuliza kilichomvutia ni mapishi au mpishi? Jibu alikuwa nalo basi? Akasema alijikuta tu yupo Tabata Kinyerezi kwa Mariam. Hakumbuki hata alipandaje gari na alifikaje!
Mshikaji wangu akaniuliza: "Hivi Wachaga na biriani wapi na wapi?" Nikamwambia ashike adabu, hao ni wakwe zangu! Hata hivyo, mimi nilijua kilichomtoa Bwa Shee Kishimundu siyo biriani la Mariam, bali Mariam Biriani. Sijui umenielewa? Namaanisha Bwa Shee alivutwa Kinyerezi na mpishi wala siyo mapishi.
Dar ina hatari Sheikh! Na wanaume wa Dar wamenishinda tabia. Dada yangu Zuwena ambaye mnamwita Shilole, si ndiye alikuwa kituo kikuu cha mahanjumati? Tukaambiwa "Shishi Food" ndiyo habari ya mjini. Siku hizi simsikii. Masikio ya wanaume Dar yameelekezwa Kinyerezi.
Kimsingi wanaume wa Dar antena zao kwa sasa zimeshategeshewa Kinyerezi. Mawimbi ambayo hunasa kichwani kwa wanaume wa Dar ni Kinyerezi, biriani na Mariam. Hupita Kinondoni kwa Shishi kama hawamjui. Shishi na umalkia wake wa nguvu aliotunukiwa juzikati na Clouds Media ni wa kuchakazwa vibaya namna hii na Mariam Biriani? Sijapenda!
Ndimi @luqmanmaloto