Baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kwamba Rais amesikitishwa na kitendo cha Bunge la Tanzania kuazimia kutofanya kazi na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Ikulu imekanusha na kudai kwamba taarifa hizo hazina ukweli.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa amesema kuwa Taarifa hizo zinazosambazwa hazina ukweli wowote na badala yake zinapaswa kupuuzwa.
Taarifa iliyokanushwa na Ikulu ilikuwa ikisema kwamba, "Ikulu inalikumbusha Bunge kwamba tayari CAG, amekwisha wasilisha ripoti yake kwa Rais hivyo inatakiwa kuja bungeni kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza. Pia Bunge litambue Mammlaka ya CAG na kwamba hawajibiki kwa Spika wala Bunge".
Taarifa hii ya kughushi imetoka siku chache baada ya April 2, 2019, Bunge la Tanzania kuazimia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG, Prof Mussa Assad kwa kutoa kauli iliyoashiria kulidhalilisha Bunge baada ya kusema kuwa Bunge ni 'dhaifu'.