Inadaiwa kuwa jana majira ya saa 11:30 jioni askari wa JKU wapatao 6 walivamia kituo cha polisi Madema wakiwa na bunduki aina ya SMG na kushinikiza kuachiwa huru askari wenzao alieshikiriwa na jeshi hilo kwa kosa la kumshambulia Askari polisi kikosi cha usalama barabarani.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja Thobias Gesauda Sedoyeka alisema tukio hilo lilitokea mara baada ya jeshi la polisi kumtia nguvuni Askari kutoka kikosi cha JKU anaejulikana kwa jina Said Kombo Abeid kwa kosa la kumshambulia askari wa trafiki siku ya tarehe 08 april mwaka huu.
“Askari hao wa JKU walikuja hapa kituoni wakiwa na bunduki aina ya SMG na kuzunguka uzio wa kituo huku wakipiga koki silaha zao na kupiga kelele kuachiwa kwa askari mwenzao” alieleza.
Alieleza kamanda mara baada ya kuona hivyo tuliwasiliana na Polisi wenzao F.F.U kwa njia ya redio na kutoa msaada na walipofika waliweza kutuliza vurugu zilizokuwa zinaendelea na kufanikiwa kuwakamata askari 6 wa JKU.