Baraza hilo limetoa siku 15 kwa Baraza la Kijeshi la Sudan kutekeleza maelekezo hayo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Waziri Mkuu anasimikwa na anatokana na matakwa ya wananchi.
Lieutenant General Jalal al-Deen al-Sheikh, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Kijeshi la Sudan amekutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia jijini Addis Ababa yalipo makao makuu ya Umoja wa Afrika, na amemueleza kuwa wanaendelea na mchakato wa kuweka utawala wa kiraia.
“Tayari tuko kwenye mchakato wa kumchagua Waziri Mkuu kwa ajili ya kuweka Serikali ya kiraia,” Shirika la Habari la Sudani (SUNA) limemkariri.
“Kwahiyo tumeanzisha mchakato huu kabla hatujakutana na Umoja wa Afrika. Huo ndio msimamo wetu na ndio njia ya kuelekea kwenye amani, lakini pia tunaheshimu na tunafuata maamuzi ya Baraza la Amani na Usalama,” aliongeza.
Wananchi wameendelea kuandamana katika mitaa ya jiji la Khartoum wakishinikiza kuwepo kwa utawala wa kiraia, baada ya kufanikiwa kushinikiza kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 30, Omar Al-Bashir.
Al-Bashir aliondolewa madarakani na jeshi la nchi hiyo baada ya kuongezeka kwa maandamano makubwa, anashikiliwa na chombo hicho cha ulinzi ambacho kimeeleza kuwa kitamfikisha kwenye mahakama za ndani ya nchi hiyo na sio Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
Al-Bashir anakabiliwa na mashtaka ya jinai kwenye mahakama ya ICC, na amekuwa akitafutwa kwa miaka kadhaa ili akajibu mashtaka dhidi yake.