Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso, amemtaka Mbunge wa Jimbo la Kibamba John Mnyika kufanya ziara katika jimbo lake ili aweze kujua ni maeneo gani yanayo pata maji ndani ya jimbo lake.
Aweso ameyasema hayo leo bungeni katika kipindi cha maswali na majibu wakati akimjibu John Mnyika aliyetaka kujua takwimu halisi ya upatikanaji wa maji katika mitaa ya jimbo la Kibamba.
Aweso alishangaa Mbunge huyo kutohafahamu mitaa ipi inayopata maji katika jimbo lake na kumtaka aongozane naye kufanya ziara ili aweze kuwa na takwimu sahihi za upatikanaji wa maji.
"Nimshauri Kaka yangu Mnyika aende Hodongo akaone utekelezaji wa mradi wa maji, aende kata ya Matosa akaone kazi kubwa inayofanywa na serikali yetu. Nipo tayari kuongozana naye nikamuonyeshe kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Anayelala na Mgonjwa ndiye mwenye kujua mihemo ya mgonjwa nakushauri nenda jimboni ukafanye ziara", amesema Aweso.
Pamoja na hayo Naibu Waziri amesema kwa sasa asilimia 80 ya wakazi wa Kibamba wanapata huduma ya maji, lakini maeneo yaliyo milimani hayana maji kwa sasa.