Lengo la hatua hiyo ni kukamata fursa iliyopo nchini, baada ya katazo la mifuko hiyo ya plastiki katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kupatikana kwa eneo hilo, kutawezesha nchi kuzalisha bidhaa hizo kwa wingi na kuuza katika soko la Afrika Mashariki, ambapo nchi wanachama walikubaliana kusitisha matumizi ya mifuko hiyo kwa lengo la kulinda mazingira.
Wakati Tanzania ikitangaza kusitishwa kwa mifuko hiyo kuanzia Juni mosi mwaka huu, nchi nyingine za jumuia hiyo ikiwemo Kenya na Rwanda, tayari zimeshachukua hatua hiyo. Uganda, Burundi na Sudan Kusini zinaendelea na michakato ya kufanya uamuzi huo.
Akizungumzia uwekezaji kwenye mifuko ya plastiki, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angella Kairuki alisema katazo la serikali kuzuia mifuko ya plastiki ni fursa kubwa kwa watanzania.
Alisema watahakikisha wanaweka makatazo mengi, hata kwa mifuko ya karatasi inayotoka nje ya nchi ili kulinda soko la uzalishaji wa ndani kwa wawekezaji watakaojitokeza pamoja na wajasiriamali.
Alitoa ombi kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuona fursa hiyo, kwa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya viwanda vya mifuko ya karatasi ili kuhakikisha ifikapo Juni 1, mwaka huu, maeneo ya uwekezaji yanakuwa yapo tayari.
Pia alitaka kutafuta fedha ili Watanzania kuwekeza katika fursa hiyo muhimu, kwa kutengeneza mifuko inayotokana na karatasi na teknolojia mbalimbali nyingine.
Kairuki alisema inakadiriwa Watanzania wanatumia mifuko bilioni tatu. Kwa wastani Mtanzania mmoja anatumia mfuko mmoja au miwili kwa wiki.