Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameendelea na ziara yake Mkoa wa Ruvuma ambapo amezungumza na wananchi na kuwaahidi kuwapatia umeme.
Akizungumza na wakazi wa Ruvuma Rais Magufuli amesema awali wananchi walikuwa wanatumia jenereta ili kupata umeme lakini kupitia mradi wa umeme wa gridi ya taifa na ujenzi Strigler Gorge utapunguza tatizo la umeme nchini.
"Tulikuwa tunatumia umeme wa jenereta ambao ulikuwa hautoshi, kwa hiyo tumeweka Megawats zaidi ya 48 ili kuwe na umeme wa kutosha sasa tunatumia Gridi ya Taifa kilichobaki ni kusambaza kwenye vijiji vyote, Dkt Kalemani wewe ni Waziri nakutaka ukafanyie kazi kwenye REA awamu ya tatu vijiji vilivyobaki vipate umeme." amesema Rais Magufuli
Awali katika tukio hilo Rais Magufuli alilazimika kuomba ridhaa ya kuvaa kofia kufuatia kuchomwa na jua kali pindi alipokuwa amesimama juu ya gari.
"Mnaniruhusu jamani nivae kofia, unajua sisi wenye vipara unatandikwa jua mpaka unajisikia mwenyewe vipi vijana mnaniruhusu?" aliuliza Rais Magufuli
"Mimi siku zote nitaendelea kuwa mtumishi wetu, suala la kupewa kazi ya urais sio kwenda kustarehe"aliongeza Rais Magufuli
Rais Dkt John Pombe Magufuli Aprili 5, 2019, alianza ziara ya kikazi ya siku 6 Mkoa wa Ruvuma akitokea mkoani Mtwara ambapo alifanya ziara ya siku 3.
EATV