Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Humphey Polepole amewakemea wanachama wa Chama hicho walioanza kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa kabla ya wakati na nje ya utaratibu.
Polepole aliyasema hayo akiwa katika ziara kukagua na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 na kuzungumza na wanachama na viongozi katika mkutano wa ndani kwenye Kata ya Goba wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Alisema si sahihi kuanza kampeni kabla ya wakati na nje ya utaratibu wa CCM. Aidha, aliongeza kuwa CCM imejipanga kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na kwakuwa itawaletea wananchi wagombea wenye sifa.
Polepole alisema pia kuwa Serikali, chini ya Rais John Magufuli imefanya kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika maeneo mengi nchini, hivyo kuwa na sababu ya kuamini kwamba itafanya vizuri katika uchaguzi huo.
"Wapo wanachama walioanza kupitapita wakitaka uongozi nje ya utaratibu wa CCM, niwaambie, wanaovunja utaratibu hatutowapitisha," alisema Polepole.