Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu amesema baada ya kuzungumza na jopo la Madaktari wake ameambiwa tarehe ambayo anaweza kuwa amepona kabisa hivyo ataweza kurudi nchini muda wowote kuanzia tarehe hiyo.
Kupitia waraka wake maalum ambao amekuwa akiutoa mara kwa mara kuhusiana na mwenendo wa afya yake Tundu Lissu amesema atakutana na Dakatri wake mara ya mwezi wa tano na kumalizia matibabu madogo ili aweze kujipanga kurudi Tanzania huku akisema tarehe hiyo hawezi kuitaja kwa sasa.
"May 14, 2019 nitapimwa urefu wa miguu ili nitengenezewe kiatu maalum kwa ajili ya mguu wa kulia, kwa sababu ya majeraha makubwa niliyopata, bila kiatu au soli maalum nitakuwa 'langara' sana na madaktari wamesema hiyo sio sawa sawa, pia nina tarehe ambayo madaktari wangu wamesema nitakuwa 'fiti' kurudi nyumbani", ameandika Lissu.
"Msiniambie niseme kwa wakati huu nahitaji kushauriana na wadau kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwangu nyumbani, Kwa hiyo, wakati muafaka utakapofika, nitawaeleza tarehe kamili ya kurudi nyumbani na kwa mlioko Dar es salaam, mniandalie supu ya utumbo wa mbuzi." ameendelea kuandika Lissu.
Kuhusiana na madai yake ya mshahara Lissu ameandika kuwa, "Spika Ndugai na watu wake wamelipa mshahara wangu wa tangu Januari hadi Machi waliokuwa wameuzuia kiharamia tu, kwa maoni yangu kilichowafanya wakubali yaishe ni ujasiri wenu, na wa watu wengine wengi, mlioamua kunichangia".
Lissu kwa sasa anapatiwa matibabu nchini Ubelgiji kufuatia kushambuliwa kwa risasi alipokuwa kwenye muendelezo wa vikao vya Bunge jijini Dodoma Septemba 2017.