RAIS wa Klabu ya Lyon, Jean-Michel Aulas ametoa taarifa kuwa klabu yake haina nafasi ya kumpa ajira kocha Jose Mourinho, mwishoni mwa msimu huu kutokana na sababu za kiuchumi.
Mourinho amekuwa hana kazi ya ukocha tangu alipofukuzwa katika timu ya Manchester United, Desemba, mwaka jana kutokana na kuwa na matokeo mabaya.
Kumekuwa na taarifa za kuwaniwa sehemu kadhaa ikiwemo Lyon ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
“Nilikutana naye mwaka jana Moscow (Urusi), tulizungumza lakini hatukujadiliana suala la yeye kuja Lyon, ukizungumzia kuhusu kumpa ajira ni suala gumu kwetu kutokana na uchumi wetu,” alisema rais huyo.
Taarifa za Mourinho ziliibuka mara baada ya kutoka kwa habari za Lyon kutokuwa tayari kuongeza mkataba wa kocha wao wa sasa, Bruno Genesio.
Licha ya kushika moja ya nafasi tatu za juu katika Ligue 1, Lyon ilifungwa mabao 3-2 na Rennes katika mchezo wa nusu fainali ya Coupe de France.