Tishio la madaktari hao limekuja baada ya mwenzao kuuawa wiki iliyopita na watu wasiojulikana ambao waliwashambulia wafanyakazi wa masuala ya afya wanaofanya juhudi za kupambana na maradhi ya Ebola.
Dakta Kalima Nzanzu mmoja wa madaktari hao amewataka wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutambua kwamba, wafanyakazi wa afya wapo mashariki mwa nchi hiyo kwa ajili ya kupambana na mardhi ya Ebola.
Aidha ameitaka serikali ya Kinshasa kuwapatia ulinzi wa kutosha madaktari wanaohudumu kwa ajili ya kutokomeza maradhi ya Ebola.
Hivi karibuni kundi la wanamgambo lilishambulia kituo kimoja cha afya huko Butembo ikiwa ni masaa machache tu baada ya shambulio jingine kama hilo lililopelekea daktari mmoja kutoka Cameroon kuuawa.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, tangu homa ya Ebola ilipolipuka tena nchini humo mwezi Agosti mwaka jana 2018 hadi sasa, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa au wanaoshukiwa kuambukizwa imefikia 1,206 , na zaidi ya 800 kati yao wamefariki dunia.
Mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.