Tabora. Watoto sita wameuawa na mwanamke aliyejulikana kwa jina la Nana Maganga, kati yao watano ni wa kwake na mmoja wa kaka yake.Mwanamke huyo ni mkazi wa kijiji cha Luzuko, kata ya Mizibaziba wilayani Nzega
Hata hivyo, mwanamke huyo naye inaelezwa akifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha huku ikidaiwa kuwa aliuawa.Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley, amesema tukio hilo limetokea jana saa 11:00 jioni.
Nley amewataja waliokufa kuwa ni mapacha Shija na Nyawele Dotto (2), Kurwa na Dotto (4), Soda Dotto (6) na Pala Masanja (3).Waliojeruhiwa ni Kundi Dotto na Nembwa Dotto, Milembe Masanja na Mwashi Masanja.
Amesema polisi inawashikilia mganga wa kienyeji Masanja Jisenge na kaka yake, Dotto Jisenge ambaye ni mume wa Nana.Wengine ni ndugu zao Mapande Kulingwa, Mafuta Tungu na Paul Penda.
Akizungumzia tukio hilo, Nley amesema Nana inadaiwa alikuwa mgonjwa wa akili na alikwenda kwa mganga wa kienyeji ambaye ni shemeji yake, Masanja Jisenge, kupatiwa matibabu ambako mkasa huo ulitokea.
Kamanda huyo amesema ndugu waliomdhibiti Nana walikana kumuua wakidai walimkamata na kumfunga kamba mikononi na kuwa kifo chake ni kutokana na kunywa sumu mwenyewe, jambo ambalo polisi ilipinga.
Mkuu wa wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla, amesema tukio hilo limeiacha jamii katika mshangao na kuwataka wananchi wanapohisi ndugu yao ana ugonjwa wa akili kumpeleke kupata tiba vituo vya afya, hospitali na zahanati.
Naye mwenyekiti wa kijiji hicho, Jilatu Lukwizu, amesema wamejifunza na wataanza kutoa elimu dhidi ya watu wanaohisiwa wamerukwa akili ili wapewe matibabu sehemu husika sio kwa waganga wa kienyeji