Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa kikosi cha Simba kinapaswa kupewa sifa yake hivi sasa badala ya kungoja miaka 20 au 30 ijayo.
Akizungumza katika mkutano wake na wanahabari, Makao Makuu ya klabu hiyo, Msimbazi Jijini Dar es salaam kuelekea mchezo wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe, Manara amesema mashabiki wengi wa Tanzania wana shida ya kutosifia vya kwao pindi vinapofanya vizuri bali hungoja hadi muda upite na kusifia wakati wenyewe hawapo.
"Simba imeweka rekodi kwa nchi kupitia hatua nyingi hadi robo fainali. Tumeanza na Mbabane Swallows, tukacheza na Nkana Red Devils halafu tukacheza mechi sita za makundi, ni rekodi kubwa. Tusichukuliane kirahisi hivi halafu baada ya miaka 20 ijayo ndo mkaanza kusifia", amesema Manara.
"Wapeni moyo watu ambao wanafanya vizuri, shida yetu baadhi ya watanzania hatupendi kusifia chetu, tumewafunga AS Vita ambao mlisema kuwa ndio wanafainali wa mwaka jana, tukawafunga Al Ahly ambao mliandika ndio klabu tajiri zaidi Afrika lakini sasahivi hawasemi", ameongeza.
Kuhusu uwezo wa timu yake kwa sasa, Manara amesema kuwa Simba haiwezi tena kuuza wachezaji kirahisi kama zamani walivyofanya kwa Mbwana Samatta ambaye alisajiliwa na TP Mazembe kwa ada ya takriban dola 100,000.
"Sisi na Mazembe sasa hivi tuko sawa, hajulikani nani atamnunua mwenzie, sisi sasa hivi tuna uwezo wa kumnunua Tresor Mputu yule staa wao. Wakati ule sisi tulikuwa chini wao walikuwa juu lakini sasahivi tuko sawa na miaka kadhaa ijayo sisi tutakuwa mbinguni wao ardhini".
Katika hatua nyingine Afisa Habari huyo ametumia mkutano huo kutangaza viingilio katika mchezo huo wa Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Jijini Dar es salaam, Jumamosi April 6. Viingilio hivyo ni Tsh. 4,000 kwa mzunguko, Tsh. 10,000 kwa VIP B, Tsh. 20,000 kwa VIP A na Tsh. 100,000 kwa Platinum.