Rais Donald Trump amezungumza kwa simu na mbabe wa kivita wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar, akimuahidi kumuunga mkono, licha ya jitihada za Umoja wa Mataifa kusitisha mapigano ya kuwania udhibiti wa Tripoli.
Katika mazungumzo hayo ya jana, Trump na Haftar walijadiliana hatua za kupambana na ugaidi na haja ya kufikia amani na utangamano nchini Libya, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.
Taarifa ya Ikulu hiyo inasema kwamba Trump alilitambuwa jukumu muhimu la Jenerali Haftar katika kupambana na ugaidi na kulinda rasilimali ya mafuta ya Libya.
Marekani inaungana sasa na Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika kumuunga mkono mbabe huyo wa kivita, ambaye mapambano yake ya kutwaa madaraka yanatishia kuirejesha tena Libya kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Ikulu ya Marekani haikusema kwa nini ilichelewa kutoa taarifa ya mazungumzo hayo ya simu kati ya Trump na Haftar, lakini wachunguzi wanasema uamuzi wa Trump kumsifia Haftar ni ushahidi wa kwa nini jenerali huyo muasi amekuwa na dhamira ya kuutwaa mji mkuu, Tripoli, unaodhibitiwa na serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, anayetambuliwa na Umoja wa Mataifa.
Kamanda huyo wa kijeshi anaunga mkono serikali hasimu ya Libya yenye makaazi yake mashariki mwa nchi hiyo na amekataa kuyatambua mamlaka ya serikali iliyo mjini Tripoli.
Siku ya Alhamis (Aprili 18), Urusi na Marekani zilipinga rasimu ya azimio la Uingereza ambalo lilikuwa likiungwa mkono na Ufaransa na Ujerumani kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka usitishwaji mapigano nchini Libya.
Urusi ilisisitiza kutokuwepo ukosowaji wowote dhidi ya Haftar kwenye rasimu ya azimio hilo, huku Marekani ikitaka ipewe muda zaid kufikiria hali ilivyo.
-DW