Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gibson Meiseyeki amezungumzia juu ya tukio la kuvuliwa Ubunge kwa aliyekuwa Mbunge mwenzake wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari licha ya yeye kulalamikiwa na baadhi ya viongozi wa serikali kutoonekana jimboni kwake, akisema kuwa hakuna cha kujifunza kwenye
tukio hilo.
Meiseyeki ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv kuelekea uchaguzi wa marudio wa kuziba nafasi ya Nassari unaotarajiwa kufanyika Mei 19, 2019 ambapo mpaka sasa vyama 6 vimejitokeza kushiriki uchaguzi huo.
Meiseyeki amesema kuwa, "suala langu mimi halihusiana sana na la Nassari, na hamna cha kujifunza. Mimi ninafahamu taratibu za Kibunge, na wanaosema sionekani ni kwa sababu natekeleza majukumu yangu niliyiowaahidi wananchi kwenda Bungeni."
"Sikuwahi kusema kazi yangu itakuwa ni kuzunguka lakini nitakuwa Bungeni kuwawakilisha na ukitaka kuamini hilo nenda jimboni, utajua nini kimefanyika miradi ya maendeleo iko mingi sana inafanyika, lakini sio siasa za kujionesha", amesema Mbunge Meiseyeki.
"Wakati Spika anatangaza orodha ya mahudhurio bungeni ukitoa Jenista Mhagama anayefuata ni mimi", ameongeza Meseyeki.
Mbunge Meiseyeki amekuwa akiingia kwenye kutupiana maneno na Mkuu wa Wilaya Arumeru, Jerry Muro kutokana na kiongozi huyo wa Serikali kudai Mbunge Meseyeki haonekani jimboni mara kwa mara.