STAA wa timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta ameweka rekodi ya kuwa kinara wa mabao kwa wachezaji wote wa Afrika ambao wanacheza Ligi za Ulaya msimu huu.
Samatta ameweka rekodi hiyo akifunga mabao 20 katika Ligi ya Ubelgiji (Jupiler) akiwafunika mastaa wakubwa wa Afrika Mohammed Salah wa Liverpool, Nicolas Pepe wa Lille na Pierre Emerik Aubameyang wa Arsenal.
Katika ligi zao hadi sasa, Salah raia wa Misri aliyepo England amefunga mabao 18, Mgabon Aubameyang anayekipiga Arsenal, England ana 17, Muivory Coast Pepe anayekipiga Ligue 1, Ufaransa amefunga 18 pamoja na Msenegal Sadio Mane aliyepo Liverpool, England aliyefunga mabao 17.
Pia Samatta amewapita Mualgeria Ishak Belfodil wa Hoffenheim ya Ujerumani aliyefunga mabao 13, Muivory Coast, Yao Gervis ‘Gervinho’ wa Parma ya Italia mwenye mabao 10, Max Gradel wa Toulouse ya Ufaransa pamoja na Francois Komano raia wa Guinea anayekipiga Bordeaux.