Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Simba, Mohammed Dewji ametoa ahadi kuwa hatua ya mwanzo ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo huko Bunju utakamilika mwezi Mei.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo April 5, Dewji amesema kuwa kuchelewa kukamilika kwa zoezi la uwekaji nyasi kwenye uwanja huo ambalo awali lilikuwa likamilike mwezi Februari kulitokana na klabu hiyo kutozipata nyasi zake bandia kwa wakati kutokana na masuala ya kisheria.
"Pia nataka nigusie suala la uwanja wetu wa Bunju. Mungu amesaidia nyasi zetu zimeshatoka na tumeshamalizana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambao walizishikilia.
Tunangoja hizi mvua zipite na baada ya wiki kama mbili hivi tuendelee na ujenzi na Mungu akipenda, Mwezi wa tano tutaanza kutumia uwanja wetu," amesema Dewji.
Dewji amesema kuwekwa kwa nyasi bandia hakumaanishi kama ndio kutakuwa ukomo wa ujenzi wa uwanja huo bali kutafuatiwa na ujenzi wa hosteli na miundombinu mingine kama kumbi za mikutano, mazoezi na mapumziko