Mradi Wa Maji Wamuweka Kikaangoni Mkurugenzi Makambako Mbele Ya Rais Magufuli

Mradi Wa Maji Wamuweka Kikaangoni Mkurugenzi Makambako Mbele Ya Rais Magufuli
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amemuagiza waziri wa maji profesa Makame Mbalawa kushughulikia mapema changamoto ya maji mjini Makambako kutokana na kuibuka kwa lalamiko la ukosefu wa maji kwa mda mrefu lililoibuliwa na mwananchi wakati akiongea na wananchi mjini Makambako.

Awali Rais Magufuli wakati akiongea na wakazi wa mji mdogo wa makambako alimruhusu mwananchi aliyehitaji kuwasilisha changamoto ya mji huo ambapo Albat Mgihilwa mkazi wa Manga amesema wamekuwa wakikosa huduma ya maji zaidi ya miezi sita mpaka sasa.

“Mheshimiwa Rais wewe ni Rais wa wanyonge na sisi tuna miaka tangu 2009 hatupati maji kila siku wageni wakiwa wanakuja wanatengeneza maji na mgeni akiondoka na maji yanakata na sasa hivi tuna miezi zaidi ya sita hatupati maji lakini ulivyoahidi unakuja wametengeneza wiki iliyopita tunaomba utusaidie”alisema Mgihilwa

Akizungumzia changamoto hiyo ya maji mkurugenzi wa mji wa Makambako Paul Malala amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo mjini Makambako hususani katika maeneo ya Makambako kutokana na kukosa uimara wa mabomba pamoja na kupasuka kwa mabomba na viungio mara kwa mara

“Kwa ujumla mradi wa Manga una matatizo kwa siku nyingi tangu mwaka 2016 nimefika hapa mradi huo ulikuwa umekamilika  lakini ulikuwa na matatizo kuanzia kwenye usanifu wake,kuna eneo la takribani km 1.6 ndio linalosumbua tumewasiliana na meneja wa maji mkoa na tumelipitia eneo hilo imeonekana liliwekewa mabomba ya p n 6 badala ya pn 10 tayari tumewasiliana na wizara ya maji ili wizara ione uwezekano wa kusaidia kwa maana hiyo mara kwa mara kuna kupasuka kwa mabomba hayo pamoja na viungio vyake”alisema Malala

Kwa upande wake mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo Mhandisi  Malisa amesema mradi wa Manga ulisanifiwa mwaka 2009 lakini chanzo cha maji kilichobuniwa kilikuwa kikikauka maji hataua iliyowalazimu kubadilisha chanzo cha maji huku gharama ya mradi ikitumia fedha ya mwanzo na kushindwa kufanikiwa kupata maji ya uhakika katika mradi huo.

Kutokana na hatua hiyo Rais magufuli amemtaka waziri wa maji kubaki katika eneo hilo ili kushughulikia tatizo hilo.

“Swala la maji hapa inaonekana kuna matatizo fedha imetolewa na ndio maana nimetolea mfano katika bilioni 117 za miradi ya maji fedha halali ni bilioni 17 na zingine zimechapwa,naona ni uongo mwingi tu mnaongea na huyu mwananchi anaongea ukweli nataka na wewe waziri ubaki hapa ushughulikie hili tatizo”alisema Magufuli

Kabla ya kuzungumza na wananchi mjini Makambako  katika ziara yake ya siku ya mwisho mkoani Njombe, Rais Mgufuli amefungua barabara ya Mafinga-Makambako-Igawa yenye urefu wa kilomita 138.7 uliojengwa kwa kiwango cha lami ya kisasa na kugharimu Bilioni 232.61

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad