Mtoto Aliyetekwa siku 198 zilizopita Apatikana, Alikuwa Amefichwa Kilakala Morogoro


Mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Princes Gate jijini Dar es Salaam, Idrissa Ally (13), aliyetekwa kwa staili ya ‘kimafia’ Septemba 26, 2018 akiwa anacheza na wenzake maeneo ya Tegeta Masaiti amepatikana jana baada ya kurudi nyumbani mwenyewe.



Tangu siku alipotekwa hadi jana alipopatikana, Idrissa amefikisha siku 198 za kuishi mbali na familia yake huku akishindwa kuendelea na masomo.

Jana jioni alirejea nyumbani  kwao na wazazi wake waliokuwa hawana hili wala lile walijikuta wakimpokea na kurejewa na furaha iliyotoweka kwa kipindi kirefu.

Idrissa alitekwa Septemba 26,2018 saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alichukuliwa na dereva mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na kumuingiza mlango wa nyuma wa gari na kuondoka naye.

Idd, baba mzazi wa Idrissa amesema jana jioni mama mzazi wa mtoto huyo, Leila Kombe  alipokea ujumbe kutoka katika namba asiyoifahamu  na kuelezwa kuhusu kutafutwa na mtoto wake.

Hata hivyo, hakuamini kwa kuwa ameshapokea ujumbe wa aina hiyo mara nyingi , kumtaka mume wake apige namba hiyo.

"Nilimpigia akaniambia yupo Ubungo na kwamba mtoto wake aliomba ampigie lakini ameshaondoka akielekea nyumbani kwao Tegeta,” amesema Idd.

Anasema hakuamini lakini kama miujiza saa moja jioni aliona pikipiki ikiingia nyumbani kwake ikiwa imempakia kijana wake.

“Bado siamini kama amerudi nyumbani, tumekuwa kwenye giza nene kwa muda mrefu," amesema Idd.

Amesema mwanaye amepungua lakini amerefuka na ana nywele nyingi, “inaonekana hakuwahi kunyoa tangu alipotekwa.”

Kuhusu uwepo wake Morogoro, amesema hivyo ndivyo Idrissa alivyomueleza kwamba katika nyumba aliyokuwa akiishi ukutani kulikuwa na maandishi yaliyosomeka ‘Kilakala Morogoro’.

Amesema Idrissa amemueleza kuwa kuna kijana mmoja alimsaidia kumtorosha, alimpatia nauli akimtaka aende Dar es Salaam kwa wazazi wake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad