Mwalimu mmoja wa shule ya Donnybrook iliyopo KwaZulu Natal nchini Afrika Kusini, amesimamishwa kazi na kufunguliwa mashitaka, kwa kumfungia mwanafunzi darasani usiku kucha, kwa kosa la kutofanya kazi za nyumbani (homework)
Msemaji wa Elimu wa KwaZulu Natal, Muzi Mahlambi, amesema kwamba Mwalimu huyo alichokifanya sio kitendo cha ubinadamu na ni kosa kisheria, hivyo wamemsimamisha kazi kuanzia Jumatano April 17, huku wakiwaachia polisi kumchukulia hatua za kisheria zaidi.
“Kama kitengo tumeshtushwa na kitendo hiki ambacho sio cha kibinadamu, na huyu Mwalimu tumemsimamisha na tumemfungulia mashtaka. Tunatarajia walimu wetu kuwa wazazi kwa wanafunzi hawa, iwapo ukifanya hivi kwa mwanafunzi wa grade 3, atakuwa akiogopa shule, tunahitajika kumsaidia mtoto kisaikolojia”, amesema Mahlambi.
Naye msemaji wa polisi wa KwaZulu Natal, Colonel Thembeka Mbele amethibitisha kufunguliwa kwa kesi dhidi ya mwalimu huyo juu ya unyanyasaji wa mtoto.
Mwalimu huyo ambaye jina lake halijawekwa wazi, alimfungia darasani mwanafunzi wa 'grade 3' mwenye miaka 8 kwa usiku kucha, kuanzia saa 8 mchana baada ya muda wa masomo kuisha, kwa kosa la kutofanya kazi aliyopewa.