Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema anayo orodha ya baadhi ya wabunge waliotelekeza watoto hivyo amewataka wahusika kulimaliza suala hilo kabla hajawataja.
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo bungeni leo wakati wa kipindi cha maswali na majibu mara baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Tauhida Galloos (CCM), aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani juu ya raia wa kigeni wanaopewa vibali vya kuja kufanya kazi nchini kwa muda na kuwazalisha watoto.
Akijibu swali hilo Lugola amesema sheria tayari ipo hivyo aliwaomba kina mama ambao wamekimbiwa wafuate sheria.
“Sheria tayari tunayo, niwaombe kina mama wote ambao wameathirika na jambo hili kwa kuwa ni la jinai waende katika vituo ambavyo vipo jirani wafungue kesi ili serikali tutumie kesi hizi kuwarejesha nchini wajibu mashtaka,” amesema Lugola.
Baada ya kujibu swali hilo, Spika Ndugai alisem; “Nakubaliana kabisa na maneno ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa asilimia 100 na mimi nishuhudie ninayo mawasiliano kadhaa ya kina mama kutoka sehemu mbalimbali za nchi wakiwalalamikia wabunge wanaume kutelekeza watoto.
“Naomba kila anayehusika na jambo hili achukue hatua ipo siku hapa nitakuja na orodha patakuwa hapatoshi hapa,” amesema Spika Ndugai.