Baada ya kiungo wa Simba Haruna Niyonzima, kuonyeshwa kadi nyekundu jana April 27, kwenye mchezo wa ligi kuu kati ya Biashara United ya mkoani Mara dhidi ya Simba, mchezaji huyo leo ameeleza kujutia kosa na kuomba msamaha.
Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda, amesema anajutia kosa alilofanya la kujibizana na mwamuzi na kupelekea kuonyeshwa kadi hiyo dakika ya 70 ya mchezo huku akikiri wazi kuwa kutolewa kwake, lilikuwa ni pigo kwa klabu yake.
”Niombe radhi kwa klabu yangu mashabiki zetu waliosafiri mpaka Mara na pia wale wote mliokua majumbani mkitizama, nilichofanya hakikuwa bora kwa ustawi wa mpira wetu samahani wote mliokwazika, tutapambana mpaka tone la mwisho kwajili ya ubingwa,” ameandika Niyonzima katika ukurasa wake wa kijamii.
Aidha, katika mchezo huo Simba iliibuka na ushindi wa magoli 2-0 yote yakifunga na nahodha wao, John Bocco na kufikisha pointi 69 katika nafasi ya pili, nyuma ya Yanga yenye pointi 74.