Ofisa oparesheni mkoa wa kipolisi wa Kinondoni ambaye ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP Gerald Ngiichi ameieleza mahakama hiyo kuwa aliamuru askari kupiga risasi hewani kwa ajili ya kutawanya maandamano ya viongozi na wafuasi CHADEMA.
Ushahidi huo ambao wa kwanza kutolewa katika kesi hiyo, SSP Ngiichi alidai kuwa aliamuru risasi zipigwe kwa sababu njia ya kutumia mabomu ya Moshi ‘Machozi’ ilishindikana kuwatanya.
"Nililazimika kutumia njia ya mwisho ya kutumia silaha za moto kupigwa hewani kutoka na waandamanaji kutotii ilani tatu nilizozitoa katika umati huo wa waandamanaji kwa kutumia kingo'ra nikiwa katika gari la polisi," alidai Ngichi.
Alidai kabla ya kutumia njia ya mwisho ya kuamuru askari wake wa vikosi vya doria kupiga risasi juu, aliamuru kikosi cha askari walikiwapo katika eneo hilo kupiga mabomu ya moshi kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wanaongozwa na viongozi wa chama hicho.
Alidai wakati askari wake wakiendelea kurusha mabomu ya moshi kwa waandamanaji hao, hawakufanikiwa vizuri kutokana na moshi wa mabomu hayo kuelekea upande walipo askari hao.
"Zoezi la kupiga mabomu waandamanaji hao lilikuwa hafifu kutokana na moshi kuelekea upande walipo askari badala ya kwenda kwa waandamanaji kutokana na upepo uliokuwapo eneo hilo hali iliyopelekea waandamanaji kutosambaratika" alidai Ngichi.
Alidai katika harakati za kurusha mabomu kwa waandamanaji hao, askari polisi wawili ambao ni PC Fikiri na Koplo Rahim waliokuwapo eneo la tukio walijeruhiwa kwa mawe na kuanguka chini.
"Baada ya kuanguka chini askari hao niliamuru askari wengine watoe msaada kwa majeruhi hao kwa kuwaondoa katika eneo hilo na niliamuru kikosi cha mabomu kirudi nyuma na kikosi cha risasi kisonge mbele ili kukabiliana na waandamanaji hao," alidai.
Alidai askari wenye silaha walisogea mbele na kupiga risasi hewani ili kuwatawanya waandamanaji waliokiwa wanataka kuchukua silaha baada ya askari wake wawili kujeruhiwa na kuanguka chini.
"Risasi zilivyopigwa hewani kishindo kulikiwa kikubwa hali iliyopelekea watu wengi kukimbia akiwamo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, sikujua kama mheshimiwa Mbowe anajua kukimbia namna hiyo," alidai Ngichi
Pia amedai, baada ya waandamanaji kusambaratika, alifanya tathmini na kubaini kuna majeruhi wawili ambapo alikuwepo Akwilina aliyewahishwa Hospitali ya Mwananyamala na baadae kuripotiwa kuwa amefariki.
Ngiichi ambaye ni Ofisa Operesheni wa Kipolisi Kinondoni, na shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka katika kesi ya uchochezi inayowakabili vigogo tisa wa chama hicho ameyaeleza hayo wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 13, 14 na 15, 2019 kwa ya kuendelea kusikilizwa.
Ofisa oparesheni mkoa wa kipolisi wa Kinondoni Atoa Ushahidi Kesi ya Freeman Mbowe na Wenzake
0
April 18, 2019
Tags