Meneja wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amesema kuwa kwa sasa hafikirii kumuacha Paul Pogba kuondoka ndani ya kikosi hicho licha ya Real Madrid kuonyesha nia ya kupata saini ya kiungo huyo.
Pogba amekuwa ni mchezaji wa mwisho kufunga bao la kawaida ndani ya kikosi hicho alilopachika katika mchezo wao dhidi ya West Ham uliochezwa Aprili 13 na tangu hapo hakuna mwingine aliyefumania nyavu, amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na timu yake kushindwa kupata matokeo.
Solskjaer amesema," Huwezi kujipa matumaini katika kila jambo hasa kwenye mpira, ninachofikiria mimi bado Pogba ana nafasi ya kubaki ndani ya timu yangu kwa sasa.
"Bado anasimama kama kiongozi hasa tukiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo hivyo ni mtu muhimu kwenye mafanikio ya Manchester United.
"Uongozi una vitu vingi na mabadiliko pia yapo kama ambavyo kwa sasa ipo tofauti kati ya wale ambao walinitangulia kuongoza timu kama Sir Alex (Ferguson), Louis Van Gaal na Joe Mourinho, tupo tofauti kabisa na siwezi kuongoza kama wao walivyofanya," amesema.
Mchezo unaofuata wa Manchester United ambayo kwa sasa ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi 64 baada ya kucheza michezo 35 ni dhidi ya Chelsea ambayo ipo nafasi ya nne baada ya kucheza michezo 35 ina pointi 67