Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa huku askari polisi mmoja akijeruhiwa baada ya kutokea kwa majibizano ya risasi katika tukio la ujambazi wilayani Kibondo mkoani Kigoma..
Inaelezwa majambazi hao walikuwa wamejipanga kufanya uporaji katika baadhi ya nyumba za wananchi wilayani Kibondo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Louis Bura, alisema juzi usiku polisi walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna majambazi walikuwa wanataka kuvamia baadhi ya nyumba.
Alisema walifika eneo la tukio na kurushiana risasi ambako askari mmoja, James Mwita (37) na mama mmoja, Sophia Dicksoni (60) walijeruhiwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Kibondo.
Alisema askari huyo alipatiwa matibabu ya awali na sasa amepatiwa rufaa kwenda kwenye matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na majeraha ya mguuni.
DC aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanayo ifanya kwa kuwa ni kazi ngumu.
Amewataka wananchi kuacha kuwaingilia katika utendaji kazi wao kwa kuwa wapo baadhi wanawakamata wakiwatuhumu kwa ujambazi lakini ndugu zao wanawatetea na kudai siyo majambanzi.
Pia aliwataka wananchi kuacha kutoka nje wanaposikia milio ya risasi kwa ajili ya usalama wao kwa kuwa ni hatari kufuata milio hiyo inaweza sababisha madhara makubwa.